Tuesday, 7 February 2017
UMUHIMU WA ELIMU
Katika ulimwengu wa sasa unaouzungumzia, manufaa ya elimu yanazidi kutambulika na kuongezeka kiasi kwamba katika mataifa mbali mbali hususan ya ulimwengu wa kwanza elimu inatazamwa kuwa ndilo tumaini la kipekee kiuchumi na kimaendeleo kwa sasa na kwa siku nyingi za usoni.
Utakumbuka kwamba uchumi wa nchi moja moja una msingi wake, mathalani hapa Tanzania kwa miongo kadhaa tunazungumza kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa taifa,kwa maneno mengine msingi mkuu wa uchumi wetu ni kilimo. Utakuwa unafahamu pia kwamba mataifa kadhaaa yaliyoendelea kiviwanda yanazungumzia uzalishaji wa viwandani kuwa ndio msingi mkuu wao kiuchumi.
Mtazamo wa kidunia sasa hivi ni kwamba uchumi wa ulimwengu hususan wa mataifa yanayoitwa yaliyoendelea unahama katika kutegemea zaidi viwanda na sekta nyinginezo za uzalishaji, tegemeo kubwa sasa ni maarifa ambayo chimbuko lake ni elimu. Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa dunia ya leo na kesho inaelekea zaidi katika uchumi wa maarifa.
Nchi za ulimwengu wa tatu, ikiwemo Tanzania yetu zimedumu katika kutegemea kilimo, zikashindwa kuingia katika uchumi wa viwanda. Kwa sasa nchi hizi zinayo fursa ya kujikwamua na kutoka katika maendeleo duni endapo zitajielekeza katika kuutafuta uchumi wa maarifa. Kwa mantiki hiyo nchi yetu inayo fursa ya kuingia katika ulimwengu wa kwanza, bila kulazimika kutafuta ufalme wa viwanda mama, yatosha tukiuendea sasa kwa udi na uvumba uchumi wa maarifa. Elimu ndio chombo pekee cha kutupeleka huko.
Kwa ufupi uchumi wa maarifa ni uchumi unaotegemea maarifa kama raslimali kuu. Unajua maliasili kama madini na ardhi ni rasilimali, fedha ni rasilimali hali kadhalika watu ni raslimali. Hizo ni raslimali zinazoshikika na kuonekana wazi . lakini maarifa ni tofauti kidogo . Vile vile wakati rasilimali hutumika na kuisha, rasilimali ya maarifa haiwezi kuisha bali huwa bora zaidi na kuongezeka kadiri inavyotumika.
Uchumi huu wa maarifa unaeleweka zaidi unapochanganuliwa katika zile zinazoitwa nguzo zake kuu nne. Hizo nguzo ni Elimu na uendelezi wa rasilimali watu; pili, Utafiti, uvumbuzi na ubunifu; tatu, Tekinolojia na mawasiliano; na nne ,ni Mfumo wa utawala na nyenzo sahihi.
Katika nguzo ya elimu na uendelezi wa rasilimali watu, ili taifa liufikie uchumi wa maarifa linatakiwa kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ina ubora wa hali ya juu na watu wa nchi husika wanaendelezwa kwa wingi, kama sio wote ili wafikie viwango vikubwa vya elimu na kuyapata maarifa watakayoyatumia kuujenga uchumi wao. Taifa halina budi kuhakikisha si tu kwamba halina raia yoyote mjinga bali pia asilimia kubwa ya raia ni wahitimu wa vyuo vikuu katika fani mbali mbali na ni wasiokoma kutafuta maarifa hata wawapo kazini na katika maisha yao yote ili wazidi kupata ujuzi wa kazi, wawe wazalishaji zaidi na washindani.
Katika nguzo ya utafiti, uvumbuzi na ubunifu taifa linatakiwa kuwa na mchakato endelevu wa kufanya tafiti zinazolenga kugundua maarifa mapya, suluhu za matatizo mbalimbali, ugunduzi wa nyenzo na uboreshaji wa zana za kazi. Tafiti za namna hiyo zitalifanya taifa kuboresha kila sekta ya uzalishaji na zaidi sana zitalinufaisha taifa kwa njia ya kuuza maarifa yaliyogunduliwa kwa mataifa mengine. Nadhani unafahamu ni kiasi gani wagunduzi wa vitu mbali mbali wanazinufaisha nchi zao kwa kile wanachokigundua. Chukulia mfano wa ugunduzi wa kupmyutai unavyozinufaisha nchi zilizogundua. Ni wazi kuwa elimu yetu inapaswa kuwa na mkono katika hili, tunatakiwa kuwa na elimu inayomfanya mwanafunzi awe na uwezo wa kutafiti na kugundua maarifa mapya au kuwa mbunifu hata akaboresha yale yaliyopo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment